Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta jana ametoa pasi ya bao la
kwanza la timu yake, KRC Genk ikifungwa 3-2 na wenyeji, Kortrijk katika
mechi ya Kombe la Ubelgiji Guldensporen mjini Kortrijk.
Samatta
alimsetia mshambuliaji Marcus Ingvartsen kuifungia bao la kwanza Genk
dakika ya 17, kabla ya kiungo Mnigeria, Abdul Ajagun kuwasawazishia
wenyeji dakika ya 23 na kiungo mwingine, Mfaransa Larry Azouni akafunga
la pili dakika ya 36.
Wakati
kipindi cha kwanza kikikaribia kabisa kumalizika, Genk wakasawazisha
kupitia kwa kiungo Mbelgiji, Thomas Buffel dakika ya 45 na ushei.
Kipindi
cha pili, wenyeji, Kortrijk wakamaliza kazi kwa lao tatu la beki
Mfaransa, Lucas Rougeaux dakika ya 88 na sasa timu hizo zitarudiana
Februari 6 nyumbani kwa Genk, Luminus Arena.
Jana
Samatta alikuwa anacheza kwa mara ya pili tangu apone maumivu ya
mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia iliyochanika Novemba 4,
mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren
katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus
Arena mjini Genk na kumsababisha afanyiwe upasuaji mdogo.
Mechi
ya kwanza ni iliyopita iliyokuwa ya Ligi, ambayo aliingia dakika saba
za mwisho kuchukua nafasi ya Mkosovo Edon Zhegrova, Genk ikilazimishwa
sare ya 1-1 na Sint-Truiden Januari 27 Uwanja wa Luminus Arena kabla ya
jana kuanza hadi dakika ya 75 alipompisha Zhegrova.
Samatta
jana amecheza mechi ya 72 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka
2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Na
katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market,
African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano
yote.
0 maoni:
Chapisha Maoni